Siku kadhaa baada ya usiri wa mazungumzo ya kutafuta suluhisho la mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar uliotokana na tangazo la kufutwa kwa uchaguzi mkuu visiwani humo, Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amepanga kuitoa siri hiyo leo.

Taarifa zilizotolewa jana na CUF kwa waandishi habari, zilieleza kuwa Maalim Seif atafanya mkutano na waandishi wa habari leo majira ya saa tano asubuhi katika hoteli ya kitalii ya Serena, ambapo ataelezea kuhusu mwenendo wa mazungumzo ya kutafuta maridhiano.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Maalim Seif ambaye alikuwa mgombea urais wa Zanzibar, kutoa tamko rasmi kuhusu mazungumzo yanayoendelea huku chama chake kikiwa tayari kimeweka msimamo kuwa hakutakuwa na marudio ya uchaguzi.

Hata hivyo, Chama cha Mapinduzi (CCM) mara kadhaa kimekuwa kikieleza kuwa mazungumzo ya kutafuta maridhiano yanaendelea vizuri huku kikiwataka wananchama wake kujiandaa na marudio ya uchaguzi mkuu siku chache zijazo.

Mazungumzo ya kutafuta maridhiano yalihudhuriwa na marais wastaafu wa Zanzibar pamoja na wanasiasa waliowahi kushika nafasi za juu katika ngazi mbalimbali za uongozi nchini.

Hivi karibuni, Rais John Magufuli alikutana na Maalim Seif na Dk. Ali Mohamed Shein (CCM) kwa nyakati tofauti na wote walieleza kuwa mazungumzo ya kutafuta muafaka yanaendelea vizuri. Kadhalika rais Magufuli alieleza kuridhishwa na juhudi zinazoendelea kutafuta maridhiano.

 

Sepp Blatter Bado King'ang'anizi
Madereva wa Mabasi Ya 'Mwendo Kasi' wapanga kuigomea serikali