Kaimu Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti na Kutokomeza Malaria Dkt. Abdalah Losasi amesema kiwango cha maambukizi ya malaria kimepungua nchini na kufikia asilimia 8.1 kwa mwaka 2022 ikilinganishwa na mwaka 2008 ilipokuwa asilimia 18.1.
Dkt. Losasi ameyasema hayo nakuongeza kuwa vifo vitokanavyo na malaria vimeshuka kwa asilimia 76 kutoka vifo 6,311 vya mwaka 2015 hadi vifo 1,502 kwa mwaka 2022 huku waliothibitishwa kuwa na malaria wakipungua kutoka watu milioni 7.7 kwa mwaka 2015 hadi watu milioni 3.5 kwa mwaka 2022.
Amesema, awali ni mikoa sita pekee iliyofanikisha kushusha kiwango cha malaria na kwasasa mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Mwanza na Songwe imefanya idadi kufikia tisa huku maeneo ya Vijijini yakiwa na maambukizi kwa asilimia 10.7 ilikinganishwa na maeneo ya mjini yenye asilimia 0.7.
Hata hivyo, amebainisha kuwa watu wenye hali duni ya maisha wamekuwa wakikumbwa zaidi na ugonjwa wa malaria kwa asilimia 14.5 huku watu wanaoishi katika makazi bora wakiwa na maambukizi kwa asilimia 0.6.