Mabalozi kutoka nchi za ulaya, waliotembelea miradi inayotekelezwa na FETA ukiwemo wa utoaji elimu ya ufugaji samaki kwa njia ya vizimba kwenye Ziwa Victoria, wamesema wameridhishwa na namna fedha walizowekeza jinsi zinavyotumika na kuhamasisha vijana kuiomba serikali iwasimamie, ili waweze kutumia kwa malengo tarajiwa.
Mabalozi hao, walikuwa wakizungumza kwa nyakati tofauti jijini Mwanza mara baada ya kutembelea miradi hiyo na wamewaasa vijana kuchangamkia fursa hiyo kwa kuanza na kidogo walichonacho, ili waweze kufikia malengo yao waliyojiwekea maishani.
Umoja wa Nchi za Ulaya umewekeza Shilingi Milioni 800 kwa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi Tanzania (FETA), kwa ajili ya kukuza Sekta ya Uvuvi kupitia ufugaji samaki ambapo wanawekeza kwenye miundombinu.
Mwingine ni katika mitaala na kuwawezesha wakufunzi kupata elimu zaidi kwenye ukuzaji viumbemaji kwa njia ya kisasa katika kipindi cha miaka minne ambapo hadi sasa mradi huo umetekelezwa kwa miaka miwili ili kuvutia tasnia ya ufugaji samaki.