Wakati Young Africans ikirejea Jumapili (Septemba 12) katika anga za Ligi ya Mabingwa Barani Afrika wameibuka na kauli mbiu ya ‘Mabingwa wamerejea’.
Msemaji wa Yanga Haji Manara ametangaza kauli hiyo leo Jumatano (Septemba 08) akisema Young Africans inarejea katika michuano iliyowapa rekodi.
Manara amefafanua kauli hiyo akisema Young Africans ndio klabu ya kwanza kuweka rekodi ya kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kama ambavyo walivyofanya mwaka 1998.
Manara ameongeza mbali na rekodi hiyo, Young Africans ndio klabu pekee yenye mataji mengi nchini kuliko klabu yoyote.
“Rekodi hizi pekee zinaiweka Young Africans mbele ya klabu yoyote kwa kuwa na makombe hakuna klabu inayoweza kupita mbele yake,” amesema Manara.
“Tunakuja sasa na kusema Mabingwa wamerejea Young Africans inakwenda kufanya makubwa tumejipanga na tuko tayari kwa vita hiyo.”
Aidha Manara amesema kwamba kuhusu viingilio bado havijawekwa wazi wakisubiri majibu ya Shirikisho la Soka Barani Afrika CAF juu ya idadi ya mashabiki watakaoruhusiwa katika mchezo huo kulingana na matakwa ya kuepuka maambukizi ya ugonjwa wa Uviko 19 (Covid 19).
“Tunaamini wenzetu wa CAF watatujibu katika muda wa ndani ya masaa 24 baada ya hapo tutajua ni viingilio gani klabu itapanga tayari kwa mchezo huo,” amesema Manara.
Young Africans imepata nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, baada ya Tanzania kufikia viwango vya kuingiza timu nne kwenye michuano ya kimataifa na kuthibitishwa na Shirikisho la soka Barani Afrika CAF.
Msimu uliopita Young Africans ilimaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wakitanguliwa na Mabingwa Simba SC, huku nafasi ya tatu ikishikwa na Azam FC na Biashara United ilimaliza nafasi ya nne, na zote kwa pamoja zitashiriki Michuano ya Kombe la Shirikisho.