Wakulima wa mbogamboga na matunda Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, wamepata fursa ya kipekee ya soko la uhakika la kuuza mazao yao kwa fedha taslimu kutoka shambani pamoja na kupata mikopo ya pembejeo, mbegu na mitaji yenye masharti nafuu.
Fursa hizo kwa wakulima zimetolewa na Kampuni ya MacLeans BeneCIBO yenye makazi yake Kigamboni jijini Dar es Salaam ambayo imefungua tawi lake wilayani Lushoto ili kuwahudumia kwa karibu wakulima wa mbogamboga na matunda wilayani humo.
Kampuni ya MacLeans BeneCIBO inajishughulisha na kusambaza vyakula kwenye makazi ya watu, ofisini, hotelini na kwenye vyombo vya usafiri vya nchi kavu, angani na majini kwa kuzingatia ubora uliokubalika kimataifa kwa gharama nafuu, kuzingatia afya na kutunza virutubisho vya asili. Aidha, kampuni hiyo ina program maalumu za kuwaendeleza wakulima ili waweze kufanya kilimo chenye tija.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa tawi lao jipya wilayani Lushoto katika kijiji cha Mnadani kata ya Malindi, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Nnala Mwakanyamale alisema kuwa lengo la kumfuata mkulima shambani ni kuhakikisha kuwa anafaidika moja kwa moja na kazi yake na kumuondolea hasara alizokuwa anazipata zilizotokana na uharibifu wa mazao, gharama za usafiri, kukandamizwa na madalali na uhaba wa masoko.
Mwakanyamale alisema kampuni hiyo imekuwa inadhamini vikundi vya wakulima kupata mikopo ya kilimo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB) ambapo imewezesha wakulima kupata mkopo wa jumla ya Sh. 119 milioni kutoka Benki hiyo.
Aidha, MacLeans BeneCIBO inafanya utaratibu na Taasisi za Mikopo kutoa mikopo ya kujikimu wakati wa msimu wa kilimo. .
“Tayari tumeingia makubaliano na kampuni ya mikopo ya Kopafasta ambayo itawakopesha wakulima fedha, pembejeo na mbegu na sisi tutachukua jukumu la kuwadhamini na kuwalipia riba ili wao warejeshe kiasi kilekile walichokopa,” Mwakanyamale aliongeza .
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Lushoto, Emmanuel Vuli aliyemuwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo katika uzinduzi huo, January Lugangika alisema kuwa wameipokea na wanaiunga mkono kampuni ya MacLeans BeneCIBO kwani kwa uwekezaji wao italeta mapinduzi ya kilimo cha mbogamboga na matunda na kukipa thamani kinayostahili katika kuhuisha uchumi wa viwanda. Aidha, aliwataka wakulima kuhakikisha wanalima kwa kuzingatia ushauri wa kitaalam ili kutoa mazao yenye ubora utakaokubalika kwenye masoko ya kimataifa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Lushoto, Lucas Shemdolwa alieleza kuwa wakulima wa vijiji vya eneo hilo walikuwa wamekata tamaa kutokana na changamoto kubwa ikiwa ni pamoja na mazao kuharibika kwa kukosa soko na matunzo pamoja na madalali walionunua kwao kwa bei kandamizi. Aliahidi kuwa Halmashauri hiyo itashirikiana na kampuni hiyo katika kuhakikisha wanatimiza lengo walilokubaliana kwa ufanisi na kuinua kipato cha wakulima.
Akizungumza kwa niaba ya wakulima wa vijiji vya wilaya ya Lushoto, Mwenyekiti wa Kikundi cha Wakulima wa mbogamboga na matunda cha MAVUMO – AMCOS, MALIKI AMILI SHEKIDELE aliishukuru kampuni hiyo na Serikali kwani wameanza kufaidika na mikopo; na wana uhakika wa maendeleo ya kiuchumi yatakayotokana na mazao yao.