Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amewataka viongozi wa Lebanon kuanza kutekeleza mageuzi kufikia Oktoba mwaka huu na kwamba iwapo rushwa itazuia mchakato huo msaada wa kifedha utazuiwa na baadaye taifa hilo kuwekewa vikwazo.
Macron ameuambia mkutano wa wanahabari mjini Beirut, kuwa viongozi wa kisiasa wamekubali kuunda serikali ya wataalamu katika wiki mbili zijazo kulisaidia taifa hilo la Mashariki ya Kati lenye mdororo wa kiuchumi.
“Kama ikifika Oktoba, na walichokiahidi viongozi wenu hakijafanyika, tutahitaji kufanya maamuzi, hii inamaanisha nini? inamaanisha hakuna kilichofanyika, kwa hiyo nitahitaji kuifahamisha jamii ya kimataifa kuwa hatuwezi kutoa msaada wetu, lakini pia nitahitaji kuwaeleza Walebanon kuwa tulikuwa tayari kusaidia lakini viongozi wenu wakaamua vinginevyo,” amesema Macron.
Shinikizo kutoka kwa Macron, ambaye amesema ataitembelea tena nchi hiyo Desemba, tayari limevisukuma vyama vikuu vya siasa kukubaliana kuhusu waziri mkuu mpya, Mustapha Adib, ambaye ametoa wito wa kuundwa haraka kwa serikali na kuahidi kuyatekeleza haraka mageuzi ili kufikia makubaliano na Shirika la Fedha la Kimataifa – IMF.
Macron aliadhimisha karne moja ya uhuru wa Lebanon kwa kupanda mti aina ya mwerezi katika msitu mmoja nje ya Beirut.