Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo amewapatia misaada mbalimbali waathirika wa mafuriko na maporomoko ya tope yaliyotokea Katesh Wilaya Hanang mkoani Manyara.
Hayo yamejiri wakati wa ziara yake ya kuwafariji waathirika wa mafuriko wanaopewa makazi ya muda katika Shule ya Sekondari Katesh pamoja na kukagua athari za maafa hayo yaliyotokea Desembea 3, 2023 kutokana na kumeguka kwa sehemu ya Mlima Hanang.
Akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Janet Mayanja pamoja na watumishi mbalimbali wa Serikali ambao wanatoa huduma mbalimbali kwa wathirika, Dkt. Jafo amesema Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imeanza kufanya tathmini katika eneo hilo.
Amesema tathmini inafanyika kuangalia ni wapi panafaa kujengwa makazi na maeneo ya huduma za kijamii ikiwemo soko ambalo limeathiriwa na hivyo kuweza kuepusha madhara yasitokee wakati mwingine.
“Mimi binafsi na familia yangu nimejitolea misaada ikiwemo mavazi haya na vifaa hivi ili kuwafariji waathirika wa maafa haya na nawaomba tuwe na subiri wakati Serikali inaendelea kuhakikisha mnarudi katika hali mliyokuwa nayo zamani,“ amesema.
Waziri Jafo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa kuweka nguvu ya kutosha kuhakikisha kila Mtanzania anapata stahiki huduma.
Katika ziara hiyo Dkt. Jafo ameambatana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NEMC Prof. Esnat Chaggu na Mkurugenzi wa Tafiti za
Mazingira wa Baraza hilo Dkt. Menan Jangu.