Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametangaza vifo vya watu 57, vilivyotokea eneo la Katesh Wilayani Hanang Mkoani Manyara kutokana na mafuriko hapo jana Desemba 3, 2023, huku akitoa maagizo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhusu hatua za kuchukua.
Rais samia ambaye yupo nje ya nchi kuhudhuria mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi, huku akiwa tayari ametangaza kufupisha muda wa kuwa katika mkutano hu ili kurejea nchini ameyasema hayo kupitia andiko lake la ukurasa wa X alilolichapisha muda mfupi uliopita.
“Mpaka sasa tumewapoteza ndugu zetu 57 katika maafa ya mafuriko eneo la Katesh, wilayani Hanang mkoani Manyara. Ndugu zetu wengine 85 waliojeruhiwa wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, Hospitali ya Wilaya ya Hanang na Kituo cha Afya Gendabi.”
Ameongeza kuwa, “Nimemuelekeza Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (Mb.) kupitia Idara ya Uratibu wa Shughuli za Maafa na Serikali ya Mkoa kuhakikisha yafuatayo, 1. Serikali igharamie mazishi ya ndugu zetu waliotutoka, 2. Serikali igharamie matibabu ya majeruhi wote, 3. Serikali iwape makazi ya muda wote waliopoteza makazi yao.”
Maagizo mengine ni pamoja na Vitengo na taasisi zetu zote za Serikali zinazohusiana na maafa kuhakikisha vinakuwepo eneo la tukio na kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha hali inarejea kawaida na kufanya tathmini ya maafa hayo, wakati Serikali ikiendelea na juhudi hizi, tuendelee kuwaweka katika dua na maombi wote walioathirika na maafa haya.