Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli ampongeza mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz kwa kuanzisha kiwanda mkoani Morogoro.
Aidha Rais Magufuli, amemshukia mbunge wa Morogoro Mjini Aziz Aboud kwa kushindwa kuendesha viwanda viwili alivyokuwa anavimiliki ambapo amesema kuwa ameshindwa kuendeleza viwanda viwili vikubwa cha Calvan na Moplo.
“Kiwanda cha Moplo kilikuwa kinahusika na mafuta ya kupikia, mimi nasema hadharani sikufichi, ulipewa viwanda tangu mwaka 1996 hadi mwaka jana walipokunyang’anya uliwanyima ajira hata wapigakura wako,” amesema Magufuli.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo, Ijumaa Februari 12, 2021 wakati wa uzinduzi wa kiwanda cha Ngozi cha ACE Leather Tanzania Limited-Kihonda, kinachomilikiwa na Rostam.
Katika maelezo yake Rais Magufuli amesema, “huu ndiyo ukweli na mimi nitabaki siku zote kusema ukweli, nasema uongo ndugu zangu? Abood amekaa na viwanda vya Moplo na Calvan kwa zaidi ya miaka 25.
“Huyu leo simpongezi ingawa jana nilimpongeza kwenye viwanda ndugu Abood hujafanya vizuri. Nikiondoka Morogoro sijasema hili nitakuwa mnafiki,” amesema Rais Magufuli.
Katika hafla hiyo Rais Magufuli amesema Kiwanda cha Calvan kiliuzwa kwa Benki ya CRDB, ambayo hata hivyo hawakukiendeleza, huku akimuagiza Waziri wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe kusimamia suala hilo na kiwanda hicho kifanye kazi.