Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza mradi wa mabasi wa Mbezi kukamilika kabla ya mwezi Novemba mwaka huu akisisitiza hakutakuwa na muda wa nyongeza na kwamba kazi ifanyike usiku na mchana ili kukamilisha mradi.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo Oktoba 8 2020, akihutubia umati wa watu waliohudhuria tukio la uwekaji wa jiwe la msingi katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Mbezi akiwa na Rais wa Malawi Lazarus Chakerwa ambaye yuko nchini kwa ziara ya siku tatu.
Aidha, amewataka watendaji waanze kujipanga vizuri kwenye matumizi ya hela na muda, na mkandarasi na mshauri wameaswa kushinda usiku na mchana katika eneo la mradi ili kuukamilisha.
“Mradi huu ulitakiwa umalizike mwezi wa saba haujamalizika, na hili lazima niliseme kwa dhati kisingizio ni Corona Virus, Mimi nataka wafanye mpaka wawe wanafia hapa na Corona jengo limalizike haraka,” amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amesisitiza kuufuatilia mradi huo ambao mkataba wake ni Billioni 71, vizuri hasa katika matumizi ya pesa na kuongeza kuwa mkandarasi anatakiwa aanze kukatwa fedha za kucheleshwa kukabidhi mradi huo.