Na Allawi Kaboyo- Bukoba.

Idara ya uhamiaji mkoani Kagera inamshikilia mtu mmoja raia wa Pakstan aliyeingia nchini kinyume na taratibu akitokea nchini Uganda baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kutangaza Tanzania ni salama na hakuna Corona.

Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari mjini Bukoba leo Oktoba 8, Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kagera Kamishina msaidizi Hamza Ismail Shaban amesema kuwa katika utaratibu wao wa kila siku wa kuhakikisha watu wanaoingia na kutoka wanakuwa ni Raia au watu wanaostahili kuwemo nchini, Oktoba 7, mwaka huu katika uwanja wa ndege uliopo Bukoba afisa aliyekuwa zamu aliweza kumkamata raia huyo  akitaka kupanda ndege kuelekea jijini Dar es salaam.

Shaban amesema kuwa raia huyo aliyetambulika kwa jina la Mohammed  Adinani Tahir aliiingia Tanzania upande wa Kagera akitokea nchini Uganda kwa kupita njia zisizo rasmi.

“Mkoa wetu kama tunavyojua unapakana na nchi mbalimbali, na ikumbukwe janga la Corona kwa nchi za Afrika Mashariki lilikuwa bado ni tatizo na nchi nyingi zilikuwa zimefunga mipaka yake na  wananchi wake walikuwa lockdown  na bwana huyu amekaa Uganda kwa takribani miezi 6 kuanzia mwezi wa tatu na amethibitisha ameshindwa kuondoka Uganda kwasababu ya lockdown na kuamua kukimbilia kwetu japo ameingia kinyemela kwa njia ambazo sio rasmi,” amesema Kamishna Shaban.

Kamishina Shaban ametumia fursa hiyo kuwataka raia wanaotaka kuingia Tanzania kufata taratibu zilizowekwa nchini na kuwataka watanzania wazalendo kuhakikisha wanawabaini watu wanaoingia nchini kinyemela na kuwatolea taarifa mahala popote watakapo waona.

“Nitoe rai kwa watanzania wazalendo kuwa wasiwe sababu ya watu ambao sio watanzania au ambao hawana vibali vya kuwa hapa nchini kuingia na kuwahifadhi badala yake watoe taarifa kwa idara ya uhamiaji au kwa viongozi wa serikali mahali walipo,” amesema Kamishna Shaaban.

“Kama tunavyojua nchi yetu tupo kwenye mchakato wa uchaguzi hivyo hatupaswi kuruhusu watu wasiokuwa raia au tusiowajua kuingia hapa pasipokujua lengo lao,” amesisitiza Kamishna Shaban.

Tushirikiane na wakenya kuombea Corona iondoke -JPM
"Corona isiwe kisingizio, mradi ukamilike kabla ya Novemba" - Rais Magufuli