Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kuwa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli atazikwa Machi 25, 2021 Chato, mkoani Geita.
Akilihutubia Taifakwa mara ya kwanza baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania, Samia ametoa ratiba ya kuagwa mwili wa Rais wa Tano wa Tanzania, Hayati Dokta John Pombe Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021.
Jumamosi Machi 20, 2021 mwili wa Hayati Dkt John Pombe Magufuli utatolewa Hospitali ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam na kupelekwa katika Kanisa la Mtakatifu Peter na kisha kupelekwa uwanja wa Uhuru.
Jumapili Machi 21, 2021 Wananchi wa Dar es Salaam wataaga mwili wa Hayati Dkt. Magufuli katika uwanja wa Uhuru na baadaye utasafirishwa kwenda Makao Makuu ya nchi, jijini Dodoma.
Jumatatu Machi 22, mwili utaagwa jijini Dodoma na kisha kusafirishwa kwenda jijini Mwanza.
Jumanne Machi 23, 2021 mwili utaagwa jijini Mwanza na baadaye siku hiyo kusafirishwa kwenda nyumbani kwao Chato, Mkoani Geita.
Jumatano Machi 24, 2021 Wanafamilia wa Hayati Dkt. Magufuli na Wanachi wa Chato na Mikoa ya Jirani watauaga mwili na Alhamisi Machi 25, 2021 zitafanyika shughuli za mazishi.
Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza siku 21 za maombolezo kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dkt John Magufuli.
Rais Samia pia ametangaza tarehe 22 ambapo mwili wa Dkt Magufuli utaagwa Dodoma na tarehe 25 ambayo ni siku ya mazishi kuwa siku za mapumziko.