Mahakama ya Katiba ya Mali imemtangaza Kanali Assimi Goita kuwa Rais mpya wa mpito kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Rais Bah Ndaw ambaye amejiuzulu.
Uamuzi huo unazidisha mkwamo ambapo viongozi wa mataifa ya Afrika Magharibi wakiwa wanajiandaa kukutana siku ya Jumapili kuzungumzia hatua ya kukabidhi madaraka, ambayo inahatarisha harakati za kuelekea kwenye demokrasia na kudhoofisha mapambano dhidi ya wapiganaji wa jihadi katika ukanda huo.
Goita alikuwa makamu wa rais baada ya kuongoza mapinduzi mwezi Agosti mwaka uliopita na kumuondoa madarakani Rais Ibrahim Boubacar Keita, Ndaw na Waziri Mkuu, Moctar Ouane ambao walishikiliwa baada ya mapinduzi hayo waliojiuzulu siku ya jumatano wakiwa bado kizuizini.
Aida Viongozi hao waliokuwa katika serikali ya mpito waliachiwa huru siku ya Alhamisi. Hayo ni mapinduzi ya pili kufanyika Mali ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
Kanali Goita ambaye aliwashutumu Ndaw na Ouane kwa kukiuka hati ya makubaliano kuhusu serikali ya mpito na kushindwa kuwasiliana naye kuhusu kufanya mabadiliko ya baraza la mawaziri na kushindwa kuituliza hali ya mambo nchini Mali, ukiwemo mgomo wa wiki iliyopita ulioandaliwa na shirikisho la vyama vya wafanyakazi.
Kanali huyo wa jeshi amesema atamchagua waziri mkuu ndani ya siku chache zijazo atatoka miongoni mwa wajumbe wa muungano wa upinzani M5-RFP, ulioongoza maadanamano dhidi ya Keita mwaka jana.