Mahakama Kuu ya Tanzania imebatilisha uamuzi wa Kamati ya Maadili ya Mawakili ambayo ilimfutia uwakili, Wakili Fatma Karume.
Mahakama hiyo imeagiza uamuzi huo uliotokana na malalamiko yaliyotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali yapelekwe kwenye kamati hiyo na Fatma apewe nafasi ya kujitetea.
Uamuzi huo umetolewa leo Jumatatu, Juni 21, 2021 na jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu, Issa Maige (Kiongozi wa jopo), Jaji Deo John Nangela na Jaji Edwin Kakolaki, kufuatia rufaa aliyoikata Karume akipinga uamuzi huo wa Kamati ya Mawakili.
Karume alifutiwa uwakili na kamati hiyo Septemba 23, 2020 kufuatia malalamiko yaliyowasilihwa kwake na Adelardus Kilangi, akimtuhumu kukiuka maadili ya taaluma kwa kutumia lugha ya kumdhalilisha wakati akiwasili hoja za maandishi katika shauri alilokuwa akimwakilisha mteja wake Ado Shaibu.
Hata hivyo, hakukubaliana na uamuzi huo badala yake kupitia kwa wakili wake Peter Kibatala alikata rufaa Mahakama Kuu Masjala Kuu na kuwasilisha hoja kadhaaa za kupinga uamuzi huo.
Mahakama kuu katika uamuzi wake imekubaliana na sababu moja tu ya rufaa hiyo ambayo imetosha kutengua uamuzi wa kamati hiyo.
Katika sababu hiyo ambayo Mahakama Kuu imekubaliana nayo, Karume kupitia kwa wakili wake alidai kuwa kamati hiyo haikuwa na mamlaka ya kusikiliza malalamiko ya Profesa Kilangi kwa kuwa ilikuwa inakiuka uamuzi wa Jaji Kiongozi.
Wakili huyo ametuma ujumbe kwenye mtandao wake wa Twitter kuwashukuru wote waliohusika kuhakikisha anapata haki yake hiyo.