Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam imeahirisha Kesi inayowakabili viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hadi Agosti 02, 2018 kwa kile kilichodaiwa kutofika kwa Freeman Mbowe pamoja na Wakili wao.
Hayo yamewekwa wazi na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Wilbard Mashauri leo Julai 31, 2018 huku akimuonya Mbowe kuacha tabia ya kutohudhuria Mahakamani mara mbili mfululizo kusikiliza kesi inayomkabili ya jinai pamoja na viongozi wengine, kwani kufanya hivyo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Akizungumza juu ya kesi hiyo Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa amedai Freeman Mbowe ameshindwa kufika kwa wakati Mahakamani hapo kutokana msafara wa kiongozi uliokuwa unapita wakati yeye akiwa yupo maeneo ya uwanja wa ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
“Kesi yetu imeahirishwa kutokana na Wakili wetu alikuwa Mahakama Kuu akisikiliza kesi nyingine kwa hiyo, kawaida Mawakili wakiwa Mahakama Kuu, Mahakama za chini huwa haziwezi kuendelea hiyo ndiyo ilikuwa sababu kubwa, viongozi wote tuliwasili Mahakamani kama ilivyotakiwa isipokuwa Mwenyekiti wetu Mbowe alichelewa tu lakini yupo mjini hapa,”amesema Msigwa
Aidha, viongozi wa CHADEMA walioshtakiwa ni pamoja na Mwenyekiti wao Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wa chama hicho Dkt. Vicent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu bara John Mnyika, Naibu katibu Mkuu Zanzibar, Salim Mwalimu.
Wengine ni Mbunge wa Tarime vijijini John Heche, Mbunge Tarime mjini Esther Matiko, Mbunge wa Bunda mjini Ester Bulaya, Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa pamoja na Mbunge wa Kawe Halima Mdee.
-
TRA yawataka wafanyabiashara kuacha kulalamika
-
Alichoandika Ridhiwani Kikwete baada ya Waitara, Julius Kalanga kuhamia CCM
-
Mahakama yalitoa MwanaHalisi kifungoni, lakutana na kiunzi kingine
Hata hivyo wote hao wanakabiliwa na mashtaka 13 ikiwemo la kufanya mikusanyiko isiyokuwa na kibali kwenye chaguzi ndogo za marudio Jimbo la Kinondoni Jijini Dar es Salaam zilizofanyika Februari 17, 2018