Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jana iliamuachia huru mtuhumiwa ambaye ni wakala wa Kampuni ya Richmond Development  LLC, Naeem Gire aliyekuwa anakabiliwa na mashtaka mawili.

Mtuhumiwa huyo aliachiwa huru na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha aliyetoa uamuzi huo baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibisha mashtaka ya kugushi na kuwasilisha nyaraka za uongo yaliyokuwa yanamkabili.

Huu ulikuwa uamuzi wa pili kutolewa na Mahakama hiyo dhidi ya mtuhumiwa huyo katika mashtaka hayo yanayomkabili.

Katika uamuzi wa awali, mahakama hiyo ilimuachia huru mtuhumiwa huyo baada ya kuonekana kuwa hana kesi ya kujibu lakini Mahakama Kuu iliamuru kufanyiwa marejeo ili mtuhumiwa ajitetee baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kutoridhishwa na uamuzi wa awali na kukata rufaa katika mahakama hiyo ya juu.

Mahakama Kuu iliamuru kesi hiyo kuendelea kusikilizwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kwamba haikuwa sahihi kumuachia mtuhumiwa bila kujitetea dhidi shtaka la kwanza na la pili. Mashtaka hayo ni kugushi na kuwasilisha nyaraka za uongo.

Hata hivyo, bado ofisi ya DPP ina nafasi ya kukata rufaa kwenye Mahakama Kuu endapo haikuridhishwa na uamuzi huo wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Sakata la ‘Richmond’ lilitikisa nchi mwaka 2008, baada ya Serikali kuamua kutafuta kampuni ya kufua umeme wa dharura ambapo mchakato huo ulipelekea kuipata kampuni ya Richmond Development  LLC. Hata hivyo kampuni hiyo ilidaiwa kuwa ni kampuni hewa.

Sakata hilo lilisababisha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Edward Lowassa baada ya Kamati Maalum ya Bunge iliyoongozwa na Dkt. Harrison Mwakyembe kuwasilisha ripoti yake.

Mradi wa Kinyerezi kuzalisha Megawati 575
Video: AG aruhusu viongozi kufikishwa kortini, Richmond yageuzwa mtaji wa kisiasa