Mahakama Kuu ya Malawi imeamuru kusitishwa kwa zoezi la kuhesabu kura za urais nchini humo hadi theluthi moja ya kura zote zitakapohesabiwa tena.
Uamuzi huo wa mahakama umekuja kufuatia malalamiko ya chama kikuu cha upinzani cha Malawi Congress Party (MCP) cha Lazarus Chakwera kufungua shauri Mahakamani kupinga matokeo ya wilaya 10 kati ya 28.
Tume ya Uchaguzi inatakiwa kutangaza matokeo rasmi ya urais ndani ya kipindi cha siku nane. Hata hivyo, Ijumaa wiki hii kilisitisha kuendelea kuhesabu kura zilizopigwa Mei 21 ili kutoa nafasi ya kuyatafutia ufumbuzi malalamiko 147 ya vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huo.
Mahakama Kuu katika Mji Mkuu wa Lilongwe imeeleza kuwa zoezi la kutangaza matokeo ya awali ya urais linapaswa kusitishwa hadi pale yatakapopitiwa upya na kuthibitishwa kupitia zoezi la kuhesabu upya kura hizo kwa uwazi mbele ya wawakilishi wa vyama vyote vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi huo.
Vyama vya siasa vimelalamika kuwa tarakimu nyingi kwenye fomu za matokeo zimebadilishwa kwa rangi maalum ya kufanyia masahihisho (correction fluid).
Msemaji wa MCP, Eisenhower Mkaka amesema kuwa waliamua kwenda Mahakamani kwa sababu kulikuwa na udanganyifu wa hali ya juu kwenye fomu za matokeo ikiwa ni pamoja na kubadili matokeo kwenye vituo husika.
Matokeo yaliyotangazwa hadi Alhamisi wiki hii, yameonesha kuwa Rais Peter Mutharika anaongoza kwa asilimia 40.9 ya kura zilizohesabiwa ambazo ni asilimia 75 ya kura zote.
Mshindani wake wa karibu, Chakwera wa chama cha MCP alikuwa na asilimia 35.44 ya kura zote na makamu wake wa rais, Chilima alikuwa na asilimia 18.