Jaji wa mahakama ya juu nchini Marekani ametupilia mbali kesi ya madai iliyofunguliwa na 50 Cent dhidi ya Rick Ross mwaka 2015.
Katika kesi hiyo, 50 Cent alikuwa anamshtaki hasimu wake huyo kwa kutumia bila idhidi yake mdundo wa wimbo wake wa ‘In Da Club’ ulioiteka dunia mwaka 2003. Rozay aliutumia mdundo huo kwenye mixtape yake ya Renzel Remixes.
50 alikuwa anadai fidia ya $2 milioni kutoka kwa Bosi huyo wa MMG.
Hata hivyo, Jaji ametupilia mbali kesi hiyo baada ya kubaini kuwa 50 Cent hana haki miliki ya wimbo huo bali unamilikiwa na lebo ya Shady/Aftermath Records, kwa mujibu wa TMZ.
Bosi wa G-Unit na Bosi wa MMG wamekuwa na historia ya bifu zito kati yao kiasi cha kusababisha vurugu zilizopelekea kusikika kwa milio ya risasi kwenye klabu moja ya usiku waliyoitembelea miaka kadhaa iliyopita.
Aidha, mwaka 2015, Mahakama ilimuamuru 50 Cent kulipa faini ya $7 milioni kwa kuweka mtandaoni video ya ngono ambayo ilimuonesha pia mama mtoto wa Rick Ross. Hatua hiyo ilimtesa 50 na kufikia hatua ya kutangaza mufilisi.