Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Wibert Chuma amewataka Mahakimu Wakazi wapya kutekeleza majukumu yao kwa haki na upendo.
Chuma, ametoa kauli hiyo hii leo Julai 20, 2022 mjini Lushoto, wakati wa mafunzo elekezi kwa Mahakimu Wakazi wapya na Wasaidizi wa Kumbukumbu ambayo yanaendelea katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama.
Amesema, “Lazima muelewe kwamba mtakwenda kufanya kazi pengine katika maeneo ambayo sio mlipozaliwa au wazazi wako wanaishi…nendeni mkatoe huduma kwa kuzingatia upendo na haki kama ambavyo mgependa Mahakimu wenzenu watoe haki na upendo katika eneo la kwenu.”
Msajili Mkuu huyo wa Mahakama pia amewataka watumishi hao kuwajali wateja wa ndani na nje wanapokuwa wanatoa huduma za haki na pindi wanapowasilikiza wanaohitaji ushauri ili kuleta ufanisi.
Hata hivyo, amewasisitiza kuonesha huduma zenye upendo kwa wahitaji, ili waendelea kuitangaza Mahakama ya Tanzania katika mazingira chanya.
Naye, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania, Beatrice Patrick amewataka watumishi wapya kuwa waatifu kazini na kwa Mamlaka zilizo juu yao ikiwemo na Serikali.
Aidha, amewakumbusha kuwa ni makosa kwa watumishi wa umma kutumia rasilimali za serikali ikiwemo magari, muda wa kuwa ofisini kwa maslahi binafsi na ni kinyume na maadili ya kazi.