Ombi la dharura la dola milioni 160 kusaidia Pakistan kukabiliana na mafuriko makubwa limezinduliwa na Umoja wa Mataifa, likilenga kuwafikia watu milioni 5.2 walio hatarini zaidi nchini humo.
Takriban watu milioni 33 wameathiriwa na mafuriko mabaya zaidi katika miongo kadhaa na zaidi ya watu 1,000, wengi wao wakiwa watoto wamekufa tangu katikati ya mwezi Juni wakati mvua kubwa zilipoanza kunyesha nchini Pakistan.
Akiongea hii leo Geneva Uswis, Msemaji wa ofisi ya kuratibu wa misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA, Jens Laerke amesema, “Pakistani inakabiliwa na mateso na kwamba watu wake wanakabiliwa na mvua kubwa za Monsoon zilizosababisha madhara ya mafuriko na athari zingine kubwa.”
Amesema, watu 500,000 waliokimbia makazi yao kutokana na mafuriko wanapata hifadhi katika kambi za misaada huku karibu nyumba milioni moja zimeharibiwa na zaidi ya mifugo 700,000 wameangamia.
Kulingana na msemaji huyo wa OCHA, mpango huo unazingatia malengo matatu muhimu ikiwemo kutoa msaada wa kuokoa maisha na uwezo wa watu kuishi, kama vile huduma za afya, chakula, maji safi na makazi.
Ameongeza kuwa, jambo jingine ni kuzuia milipuko mikubwa ya magonjwa ya kuambukiza kama kipindupindu na kusaidia watoto wadogo na mama zao kwa lishe na kuhakikisha watu wanapata usaidizi na ulinzi kwa njia ambayo ni salama na yenye heshima, pamoja na ufuatiliaji wa familia zilizopotezana.
Kwa upande wake, Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR), Matthew Saltmarsh amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwamba hadi sasa, hatua za shirika hilo zimelenga kuto msaada wa dharura kwenda katika maeneo yaliyoathirika.