Kiongozi mkuu wa Afghanistan, Hibatullah Akhundzada amewaamrisha majaji nchini humo kutekeleza kikamilifu sheria za Kiislamu zinazojumuisha kuuwawa hadharani, kupigwa mawe, kuchapwa, na kuwakata mikono wezi.
Msemaji mkuu wa Taliban, Zabihullah Mujahid ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, amri hiyo ya lazima iliyotolewa na Akhundzada, inakuja baada ya kiongozi huyo msiri kukutana na kundi la majaji.
Hata hivyo, Mujahid hakupatikana ili kuzungumzia zaidi kuhusu ujumbe wake huo wa mtandao wa Twitter na Akhundzada ambaye hajapigwa picha hadharani tangu Taliban iliporudi madarakani mwezi Agosti mwaka uliopita, anaongoza kwa kutoa amri na maamuzi akiwa katika mji wa Kandahar, ambao kundi la Taliban lilianzishwa.
Mapema hivi karibuni, Kundi la Taliban liliahidi kwamba litakuwa na sheria zisizo kali, ikilinganishwa na muhula wake wa kwanza wa uongozi kati ya mwaka 1996 na 2001, lakini mara kwa mara wamekuwa wakikiuka haki na uhuru wa raia wa Afghanistan.