Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa mkoa wa Tabora wawapeleke watoto wao shule na waache kuwatumia kama vibarua kwenye mashamba ya tumbaku.
Majaliwa amesema hayo wakati akizungumza na watumishi wa idara za kilimo na ushirika na viongozi wa wilaya ya mkoa huo kwenye kikao alichokiitisha ili awape maagizo maalum.
“Ninasisitiza kuanzia sasa jamii iwapeleke watoto shule kuanzia elimu ya awali hadi sekondari na tuache kuwatumia watoto wadogo kama vibarua kwenye mashamba ya tumbaku. Wakuu wa wilaya simamieni eneo hili la kuondoa watoto kwenye ajira,” alisema.
Aidha, Majaliwa amewataka viongozi wa mkoa huo wasimamie elimu ya mtoto wa kike na kuhakikisha kuwa wanahitimu elimu ya sekondari. “Kuna tatizo la mimba kwa watoto wa shule. Eneo hili pia linahitaji usimamizi ili kuwalinda watoto wa kike wamalize elimu yao. Tuwalinde wanaposoma elimu ya msingi na sekondari, wakishafika vyuo vikuu watakuwa wamepevuka na kuweza kufanya maamuzi ya kujilinda,” amesema.
Pia, amewaasa vijana wa kiume wasithubutu kuwaoa mabinti wanaosoma, kwani kwa kufanya hivyo, wataishia kufungwa jela miaka 30, amewaasa wazazi wanaoamua kuwaoza mabinti zao ili wapate mahari, nao pia wana hatari kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 endapo watabainika kushirikiana na waoaji.