Aliyekuwa mgombea Urais wa Kenya, Raila Odinga amewataka wafuasi wake kutulia majumbani na kwamba wasubiri neno lake atakalolitoa kesho.

Raila ameyasema hayo jana alipokuwa katika eneo la Kibera jijini Nairobi akizungumza na wafuasi wake kuhusu matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi ya IEBC, yaliyompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta.

Mwanasiasa huyo ambaye aliwataka wafuasi wake kususia kwenda makazini leo, alilituhumu jeshi la polisi kwa kile alichodai kuwa linawaua wafuasi wa NASA wasiokuwa na hatia.

“Sitaki kuzungumza mengi leo, nataka mtulie majumbani kwenu, Jumanne nitazungumza rasmi kuhusu mambo haya yanayoendelea,” alisema Raila.

Hata hivyo, tamko hilo la Raila liliwaibua wafuasi wake ambao waliongezeka kuingia barabarani wakikabiliana na jeshi la polisi na watu wanaounga mkono umoja wa vyama vya Jubilee.

Raila pia alitembelea eneo la Mathare na kufika katika familia ambayo msichana wa miaka tisa aliuawa kwa kupigwa risasi bila kukusudiwa. Inadaiwa kuwa mtoto huyo alikuwa akicheza katika eneo la nyumba yao kabla ya kufikiwa na risasi ambayo haikukusudiwa kumfikia.

Tume ya Haki za Binadamu ya Kenya (KNCHR) imeeleza kuwa watu 24 wameuawa kwa kupigwa risasi kutokana na vurugu hizo, huku NASA wakidai ni watu 100 na kwamba baadhi yao wamekuwa wakifichwa kwenye magunia ili wasionekane.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi la Kenya limekanusha taarifa hizo za vifo zilizotolewa na KNCHR na NASA.

Mkuu wa Jeshi la Polisi la nchi hiyo (IGP), Joseph Boinett  amesema kuwa jeshi la polisi limewaua watu sita pekee ambao walikuwa wana silaha za moto wakijaribu kuwashambulia polisi. Alisema watu hao walikuwa wahalifu wenye silaha waliowalenga polisi.

Aidha, IGP Boinett amesema kuwa jeshi hilo linaendelea kufanya upelelezi dhidi ya watu wanaochochea vurugu nchini humo ikiwa ni pamoja na kutumia mitandao ya kijamii.

“Tunachunguza idadi ya watu ambao wanatuhumiwa kwa kujihusisha na uchochezi moja kwa moja au kupitia mitandao ya kijamii. Watuhumiwa wote watakamatwa na kufikishwa mahakamani,” IG Boinett anakaririwa na ‘Citizen’.

Viongozi wa dini na serikali pamoja na vyombo vya usalama vya Kenya vimeendelea kuhubiri amani nchini humo kuepusha vurugu.

Kenya ilifanya uchaguzi mkuu Agosti 8 mwaka huu ambapo matokeo yaliyotangazwa na IEBC yalionesha Kenyatta akiwa na zaidi ya asilimia 54 dhidi ya Raila ambaye alipata asilimia 44.

Mzee wa Upako ampiga tafu Q chillah
Bunge la Iran latenga mabilioni kuboresha silaha za nyuklia