Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewasisitiza wabunge na wananchi kushiriki katika michezo ili kuipa miili yao nguvu na uwezo wa kutekeleza majukumu ya kikazi.
Majaliwa ameyasema hayo, wakati akizungumza na wabunge, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Watumishi wa Bunge na maafisa wa Serikali walio shiriki Bunge Bonanza, lililofanyika jijini Dodoma.
Amesema, ”Michezo ni muhimu kwani inatufanya tuwe na afya bora na kuimarisha undugu, kujenga urafiki pamoja na kukuza vipaji. Nampongeza Spika Dkt. Tulia Ackson kwa ubunifu huu wa kuanzisha Bunge Bonanza, ambalo litakuwa linafanyika mara kwa mara.”
Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Dkt. Tulia amesema Bunge Bonanza litakuwa linafanyika mara nne kwa mwaka lengo likiwa ni kuhamasisha wananchi umuhimu wa kushiriki katika kufanya mazoezi ili jamii iweze kuwa na afya bora zaidi.
Naye Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na Katibu wa Michezo wa Baraza hilo, Nassor Salim Ali ambaye amemuwakilisha Spika wa Baraza la Wawakilishi amesema, baraza wataendelea kushirikiana na Bunge ili kudumisha undugu kupitia michezo pamoja na shughuli mbalimbali wanazozifanya.
Mwenyekiti wa Bunge Bonanza, Festo Sanga alisema pamoja na mambo mengine bonanza hilo limeanzishwa ili kumuunga mkono Rais Dkt. Samia ambaye amekuwa akiihamasisha jamii kushiriki katika kufanya mazoezi kwa ajili ya kuupa mwili afya na kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza.