Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Bonde la Wami Ruvu pamoja na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar Es Salaam (DAWASA), kuendelea na tafiti ili kubaini maeneo yenye maji mengi na kuchimba visima kisha kuyaingiza katika mfumo wa matumizi ya kijamii.
Majaliwa ametoa agizo hilo hii leo Novemba 10, 2022 wakati akikagua visima eneo la Tabata Relini na Mwananyamala Komakoma jijini Dar es Salaam ambapo pia alishuhudia uzibuaji na usafishwaji wa kisima na zoezi la usambazaji wa huduma ya maji huku akisema zoezi hilo linatakiwa kuwa endelevu.
Aidha, Majaliwa pia amewataka Wananchi wananchi kuendelea kulinda maeneo yote yenye vyanzo vya maji, sambamba na kuyatumia vizuri maji yanayopatikana, ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa maji na kusema, “Serikali inatekeleza kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma hiyo karibu na maeneo yao ya makazi.”
Visima hivyo vilivyokaguliwa, ni miongozi mwa visima 197 vilivyochimbwa na Serikali Mkoani Dar es Salaam ambapo kati ya hivyo, 160 vimefufuliwa na kutoa lita milioni 29.4 kwa siku, huku vikiunganishwa katika mfumo na hivyo kupunguza changamoto ya maji inayotarajiwa kuondolewa kwa mikoa yote nchini.