Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaagiza Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri kuhakikisha wanaongeza udhibiti wa matumizi ya mapato katika Halmashauri wanazoziongoza.
Majaliwa ameyasema hayo hii leo Juni 28, 2022 wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya Mameya na wenyeviti wa Halmashauri zote nchini.
Amesema kumekuwa na ubadhilifu wa fedha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, hivyo ni wajibu wa mameya na wenyeviti wa Halmashauri kudhibiti upotevu wa mapato katika Halmashauri zao.
“Nawasihi kuwa makini katika kusimamia ukusanyaji wa mapato na matumizi yake katika Halmashauri mnazoziongoza, ili fedha zinazopatikana ziweze kutatua kero za Wananchi” amesema Waziri Mkuu.
Katika hatua nyingine, Majaliwa amewagiza viongozi hao kuhakikisha wanasimamia utawala bora na sheria kwenye maeneo yao ili kusaidia utatuzi wa migogoro iliyopo na kuwashirikisha wale wanounga mkono shughuli za kimaendeleo.
Aidha, amewataka kuhakikisha wananchi wanapata taarifa ya utekelezaji wa mipango na bajeti inayotekelezwa kwenye Halmashauri kwa kutumia mikutano ya vijiji ili wajue jinsi wanavyoweza kunufaika na bajeti.
Waziri Mkuu, pia amewataka kuyatumikia makundi ya jamii wakiwemo vijana, wazee na makundi maalum kwa kuwashirikisha na kuwahudumia ili kutoa fursa ya kushiriki na kuleta maendeleo.
“Jikiteni katika kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani na fedha zinazotolewa na Serikali na kubuni vyanzo vipya vya mapato kwa kuwa nyie ndio wenye fursa ya kujua maeneo yatakayoibuliwa kuongeza vyanzo vya mapato,” amesisitiza.
Aidha, amewahimiza Mameya na wenyeviti wa Halmashauri kuhakikisha wanasimamia matumizi ya fedha katika Halmashauri zao ili kuweza kujua matumizi sahihi na kuhakikisha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.