Ili kuimarisha mifumo ya Serikali katika sekta ya Afya, Wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), katika sekta hiyo nchini kote wametakiwa kujiwekea mikakati madhubuti.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe ameyasema hayo hii leo Juni 28, wakati akifungua kikao kazi cha wataalamu wa TEHAMA, kutoka katika taasisi zote za Wizara ya Afya Mkoani Morogoro.

Amesema, wataalamu hao wanatakiwa kupeana uelewa juu ya mifumo inayotumika kuhakikisha wagonjwa wanahudumiwa kwa wakati, kuweza kuangalia ripoti kwa urahisi, kuhakikisha mifumo imesajiliwa na kuangalia usalama wa taarifa za Serikali.

“Lengo la kukutaka kwetu ni kupeana uelewa wa mambo mbalimbali yaliyoainishwa na kuhakikisha tunafanyia kazi taarifa ya mkaguzi mkuu wa Serikali CAG.” Amesema Dkt. Shekalaghe

Aidha, amewataka wataalamu hao kuandaa maazimio yatakayoonesha mikakati, malengo na changamoto zote kisha waziwasilishe kwake ili maazimio hayo yafanyiwe kazi.

“Mambo muhimu ya kuzingatia ni pamoja na kuweka mkakati mzuri wa kuwahudumia wagonjwa kwa haraka na kwa muda mfupi pia tarifa zipatikane kwa wakati pindi zinapohitajika na pia ijulikane wanaolipa hapo hapo na wanaotumia Bima ya Afya,” amesema.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA Wizara ya Afya, Silvanus Ilomo amemshukuru Naibu Katibu Mkuu huyo kuwafugulia kikao kazi na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo aliyoyatoa.

“Baada ya Kikao kazi hiki tutahakikisha wataalamu wanapata uwelewa zaidi juu ya uboreshaji wa mifumo ya TEHAMA ili kufikia malengo tuliyojiwekea na bahati nzuri yamefikia katika hatua nzuri.” ameainisha Ilomo.

Amesema, watayatengenezea mkakati maagizo hayo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wagonjwa na kufanikisha utekelezaji wake, huku kikao kazi hicho, kikihunduriwa na Viongozi kutoka Wizara ya Afya, Mabaraza ya Kitaalamu na Taasisi.

Majaliwa 'awafunda' Mameya, Wenyeviti  Halmashauri
Wananchi kupewa ufahamu mipaka ya Vijiji na Hifadhi