Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limempitisha Mbunge wa Ruangwa,Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu.
Akitangaza matokeo ya kura zilizopigwa na wabunge 350 , Spika wa Bunge Job Ndugai amesema Majaliwa amepigiwa kura 350 na hakuna kura iliyoharibika hivyo amepitishwa kwa asimilia 100%
Hii ni baada Rais, Dkt. John Magufuli, kupendekeza jina la Mbunge huyo wa jimbo la Ruangwa kwenye nafasi hiyo.
Aidha baada ya Bunge kuthibitisha uteuzi wake,Majaliwa ametoa shukrani kwa Rais Magufuli pamoja na wabunge kutokana na imani waliompatia.
“Jambo hili si dogo, namshukuru sana kwa imani yake kubwa aliyonayo juu yangu nakuendelea kuniamini ” amesema Majaliwa.
Majaliwa anakuwa Waziri Mkuu kwa kipindi cha pili kuanzia 2020, baada ya kipindi chake cha kwanza (2015-2020) kumalizika Novemba 5, 2020.
katika hatua nyingine Bunge limempigia kura Mbunge wa Mbeya Mjini, Dkt. Tulia Ackson kuwa Naibu Spika wa Bunge baada ya kupata kura 350 kati ya kura 354 zilizopigwa.
Akizungumza baada ya kuapishwa kuongoza kiti hicho Dkt. Tulia amewahidi kuwa mfano wa viongozi bora.
“Asanteni sana kwa kura nyingi mlizonipa, wote tungeweza kuwa kwenye nafasi hii ambayo mimi mmeniheshimu siyo kwamba mimi ni bora lakini ni wazi mimi mmenitanguliza mbele yenu na nitajitahidi kuwa wa mfano huko mbele mlikonitanguliza” amesema Tulia.
Hiki ni kipindi cha pili kwa Tulia Ackson kushika nafasi ya Unaibu spika .baada ya kuwa katika nafasi hiyo mwaka 2015 hadi 2020.