Jumamoja baada ya kiungo mkabaji Abdulhalim Humud kutangaza kujiondoa kwenye kikosi cha Majimaji, hatimaye klabu hiyo imetoa jibu kumuhusu .
Humud, kiungo wa zamani wa Simba na Coastal Union alisajiliwa na Majimaji mwanzoni mwa msimu huu wa 2017/18 lakini hakudumu muda mrefu na ikaelezwa kuwa ameondoka kutokana na kutokuwa na maelewano mazuri na uongozi wa Majimaji.
Akizungumzia juu ya hali hiyo, Ofisa Habari wa Majimaji, Onesmo Ndunguru, ambaye timu yake inadhaminiwa na Kampuni ya Sokabeti inayojihusisha na michezo ya kubashiri matokeo, alisema ni kweli Humud hayupo lakini yeye mchezaji ndiye ambaye aliyeomba kuachwa kutokana na sababu za kifamilia.
“Humud ni kweli hatutakuwa naye, hiyo ni rasmi, yeye ndiye aliyeandika barua ya kuomba kuondoka Majimaji, alisema ana matatizo ya kifamilia na hataweza kuwa mbali na familia yake.
“TFF wameshaandika barua kwa Majimaji na Majimaji imeshajibu kwa kutoa barua ya kumuacha na kilichokuwa kimebakia ni kupatiwa haki zake,” alisema Ofisa Habari huyo.
Majimaji ambayo inashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara ina mkataba wa mwaka mmoja na Sokabet, mkataba uliosainiwa hivi karibuni.
Kampuni ya Sokabet imekuwa chaguo la washiriki wengi wanaobashiriki matokeo tangu ianze kufanya kazi miezi kadhaa iliyopita na humo ndani washiriki wanaweza kushinda hadi shilingi milioni 100.