Na Abdul Mkeyenge
NIMEITAZAMA Singida United. Nimeitazama Taifa Stars na sasa naitazama Zanzibar Heroes kule Kenya, kote huko namuona kijana mmoja wa kuitwa Mudathir Yahya akifanya kazi ya kiume katikati mwa uwanja.
Mudathir anapokuwa katika ubora huu, ni ngumu kumzima. Aliwahi kuniambia moja ya rafiki zangu ambaye kesho anakutana uso kwa uso na Mudathir katika mchezo wa Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes. Natamani kuiona mechi hii nimuone rafiki yangu akipambana na Mudathir. Natamani sana.
Nimemfahamu Mudathir miaka sita iliyopita alipokuja Dar es Salaam kushiriki michuano ya Copa Coca Cola na timu yake ya Mjini Magharibi, mimi nikiwa moja ya watu wa benchi la ufundi timu ya Mkoa Kinondoni.
Katika mazoezi ya timu zote zilizokuja Dar es Salaam kushiriki michuano hiyo, mazoezi yalikuwa yakifanyika Uwanja wa Tamco. Uwanja huo ulikuwa kama jiji la Rio de Janeiro kutokana na vipaji vingi. Pira jingi lilipigwa na kila timu katika uwanja huo.
Mjini Magharibi walikuwa na Mudathir pamoja na namba nane wake niliyemsahau jina. Huyu namba nane wa Mudathir alikuwa hatari sana, sijui hata aliko. Morogoro walikuwa na Aishi Manula, Miraji Adam. Kilimanjaro walikuwa na Farid Mussa na Kelvin Friday. Kinondoni tulikuwa na Shabalala, Joseph Kimwaga, Raymond Ngungila, Clever Mkini. Nadhani kuna picha umeipata hapo. Watu wote hawa wanakutana uwanja mmoja kwa mazoezi. Acha tu!
Mudathir alianza kunivutia huku. Alikuwa mtu wa shoka kweli kweli kama alivyo sasa. Lakini hivi sasa mwili na akili yake imekuwa kubwa zaidi ya wakati ule ambao baada ya michuano ile kumalizika jina lake lilikuwa moja ya majina waliounda timu bora ya mashindano.
Safari yake ilianzia hapo. Safari yake Zanzibar sijui. Azam FC walimsajili yeye pamoja na kina Aishi na vijana wengi. Maisha yake ndani ya Azam FC yalikuwa mazuri kwa kupandishwa timu kubwa na kufanya mambo. Hapo ndiyo wengi walianza kumfahamu.
Msimu uliopita haukuwa mzuri kwake. Muda mwingi aliishia kukaa benchi, moja ya rafiki zake wa karibu aliniambia majeraha nayo yalichangia Mudathir kuwa vile alivyokuwa.
Msimu huu ameibukia Singida United. Balaa lote hili analotuonyesa uwanjani ni mchezaji wa mkopo akitokea zake Azam FC. Kuna kitu cha kujifunza hapa kwa marafiki zangu wanaotolewa kwa mikopo katika timu nyingine.
Ndani ya Singida United amepiga mpira mwingi unaomvutia kila mmoja. Hans Van Pluijm hajampa tambala la unahodha kwa sababu yeye mchezaji wa Azam FC. Amempa kitambaa kwa kazi iliyotukuka uwanjani.
Haitokei mara nyingi kwa mchezaji aliyeko kwa mkopo kufanya kama anavyofanya Mudathir. Rafiki zangu wengi waliotolewa kwa mkopo walijikatia tamaa mwisho wa siku wakaachwa kabisa. Lakini Mudathir ametupa maana tofauti ya mchezaji wa mkopo.
Kutolewa kwa mkopo kwa mchezaji hakuna maana mchezaji hatakiwi, ameshuka kiwango au hana thamani klabuni. Angalau Mudathir amekuja na mtazamo tofauti juu ya mchezaji wa mkopo. Rafiki zangu nisiyohitaji kutaja majina yao wajifunze kitu hapa.
Kufikia mwishoni mwa msimu huu, Mudathir itakuwa moja ya bidhaa itakayopatikana sokoni kwa fedha nyingi. Alichokifanya Singida United katika muda wake wa mkopo ndicho kitakachompa fedha hizo ambazo si chini ya Sh. Milioni 50. Nani kaona hii?