Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman amesema Zanzibar ina amani na watu wake wanaishi kwa kuwasikiliza viongozi wao hasa kwenye masuala ya kisiasa, tofauti na ilivyokuwa baada ya uchaguzi wa 2015.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Dar24 Media ofisini kwake visiwani humo, Othman amesema katika kipindi kama hiki miaka iliyopita wananchi hawakuwa na uhakika na amani na usalama wao.
“Hali ya kisiasa kwa Zanzibar imetulia, ni nzuri… kwa sababu tumezoea miaka ya nyumba kipindi kama hiki, watu walikua wanalalamika hawana uhakika wa amani na usalama wao. Baada ya uchaguzi mambo yalikua hayatulii,” Makamu wa Kwanza wa Rais ameiambia Dar24.
Ameongeza kuwa utulivu uliopo visiwani humo ni jitihada za Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi na Hayati Maalim Sheikh Shariff Hamad ambao waliamua kuweka kando tofauti zao za kisiasa na kukubaliana kuleta amani kwa ajili ya wananchi, hatua iliyofanya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kufanikiwa.
Ameongeza kuwa hata baada ya Maalim Seif kufariki dunia, taharuki ya kumpata kiongozi mwingine atakayeongoza upande wa ACT Wazalendo kwenye SUK imeondoka na mambo yanakwenda vizuri na watu wana matumaini.
Angalia mahojiano kamili na Dar24 hapa: