Mtu mmoja mwenye umri wa miaka 18 aliyejihami kwa silaha nzito amewaua wanafunzi 19 wenye umri kati ya miaka 7-10 wa shule ya Msingi Robb Kusini mwa Texas nchini Marekani, pamoja na walimu wawili waliokuwa shuleni hapo.

Gavana wa Texas, Greg Abbott amesema mauaji hayo yalitekelezwa Mei 24, 2022 saa 11:32 asubuhi ambapo mshukiwa huyo kabla ya kuuawa na polisi aliwajeruhi kwa risasi askari wawili. Imeelezwa kuwa kaba ya kufika shuleni hapo alikuwa amemuua bibi yake nyumbani.

“Ni tukio la kuhuzunisha tumepoteza watoto wasio na hatia wa umri wa kuanzia miaka 7 hadi 10 na hatujui sababu ya mauaji haya alikiwa akipita darasa kwa darasa kiukweli moyo wangu umepondeka,” amehuzunika Gavana Abbott.

Amesema shambulio hilo limetokea katika Shule ya Msingi ya Robb ya Mji wa Uvalde wenye wakazi wengi wa Kilatino na linakuwa ni tukio jingine la mauaji ya idadi kubwa ya watu katika uvamizi wa shule. Desemba 2012 mtu mwenye bunduki aliwaua watoto 20 na watu wazima sita katika Shule ya Msingi ya Sandy Hook Newtown nchini humo.

Kwa upande wake Seneta wa serikali Roland Gutierrez amesema Polisi walipata taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuwa linaweza kutokea shambulio na akatoa tahadhari.

“Nilipewa taarifa na Polisi kuwa kuna chapisho la mtu akitahadharisha kuwepo kwa shambulio na alipendekeza watoto wawe waangalifu,” amedokeza Gutierrez.

Mauaji hayo yametokea ikiwa zimepita siku 10 baada ya watu 10 kuuawa katika mtaa wa watu weusi (Buffalo New York) na Mamlaka nchini humo imemshtaki mtu mmoja (18), ambaye walisema alisafiri mamia ya miili hadi eneo hilo na kufyatua risasi zilizoua na kujeruhi katika duka la mboga.

Awali msemaji wa idara ya usalama ya Umma eneo la Texas Travis Considine akizungumzia mazingira ya tukio hilo aliwatahadharisha wakazi kuwa makini na mtu yeyote wanayemtilia mashaka na kutosahau matumizi ya simu namba 911 kwa ajili ya msaada na taarifa.

Marekani, mwaka 2018 mtu mwenye bunduki aliwaua kwa risasi watu 10 katika Shule ya Upili ya Santa Fe katika eneo la Houston ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya hapo ambapo mtu mwingine mwenye bunduki aliwaua zaidi ya watu 24 wakati wa ibada ya Jumapili katika mji mdogo wa Sutherland Springs uliopo Texas.

Mwaka 2019, mtu mwingine pia mwenye bunduki katika Walmart huko El Paso aliwaua watu 23 katika shambulio la ubaguzi wa rangi.

Rais Joe Biden ameamuru bendera kupepea nusu mlingoti hadi Mei 28 kuomboleza mauaji hayo ya watu 21.

Othman Masoud aeleza kinachoendelea Zanzibar kisiasa (Video)
Habari kuu kwenye magazeti ya leo Mei 26, 2022