Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango ametembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inaotekelezwa katika Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma.
Dkt. Mpango amekagua ujenzi wa barabara ya Buhigwe – Muyama – Kasumo, na kusema barabara hiyo ni jitihada za serikali katika kuufungua mkoa wa Kigoma na kuunganisha na mikoa mingine pamoja na nchi jirani hivyo kuchochea biashara na ukuaji wa uchumi kwa wananchi.
Kufuatia hatua hiyo, amewataka viongozi wa chama na serikali katika mkoa huo kuwa na ushirikiano ili kufanikisha miradi kwa haraka zaidi na kwa ufanisi na huku pia akiwataka wananchi kutambua gharama za maendeleo ni pamoja na kujitoa hivyo wanapaswa kuunga mkono tathimini na fidia zitakazotolewa na serikali kupisha ujenzi wa mradi huo.
Aidha, Makamu wa Rais pia amekagua ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Kasumo na nyumba za wahudumu wa afya wa zahanati hiyo, mradi unaotekelezwa kwa nguvu za wananchi kwa kushirikiana na serikali.
Amewapongeza wananchi wa Kijiji hicho, kwa kujitolea kuongeza eneo la zahanati hiyo pamoja na kutoa mchango wa hali na mali katika utekelezaji wa mradi huo na kuwaasa kuendelea kutoa mchango wao katika miradi mingine.
Hata hivyo, amesema Serikali itafanya ukarabati wa nyumba za walimu katika shule ya msingi Lemba iliopo jirani na zahanati hiyo ambayo inakabiliwa na changamoto ya uchakavu kwa muda mrefu.