Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amewataka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kikosi namba 834 Makutupora kilichopo mkoani Dodoma kupanda miti pembezoni mwa barabara ya kuingia jiji la Dodoma ili kuhifadhi mazingira pamoja na kupendezesha eneo hilo.
Ameyasema hayo alipotembelea eneo hilo la JKT Makutupora, huku akisisitiza uwepo wa kambi hiyo ya jeshi katika eneo hilo ni kwa sababu ya ulinzi wa chanzo cha maji katika bonde la mzakwe hivyo wanapaswa kufanya uhifadhi huo kikamilifu.
Aidha Makamu wa Rais Dkt Mpango amewataka JKT Makutupora kuhakikisha wanadhibiti waharibifu wa mazingira na waoingiza mifugo na kuchoma mkaa jirani na chanzo cha maji mzakwe. Amesema serikali imeweka mkazo katika uhifadhi wa mazingira na tayari imeleekeza upandaji miti katika ngazi za kaya ambapo kila kaya inapaswa kupanda miti mitatu hadi mitano kulingana na maeneo husika.
Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Brigedia Jenerali Rajabu Mabele amesema JKT itatekeleza kikamilifu maagizo hayo na kuweka mkazo katika uhifadhi wa eneo hilo na sehemu zinginezo zinazohusika na JKT.