Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewaomba viongozi wa Dini kuendelea kuamrisha mema na kukataza mabaya kwani kufanya hivyo kunaipunguzia Serikali mzigo.
Makonda amesema hayo wakati akifungua semina wa Walimu wanaosomesha Qur-an Tanzania (JUWAQUTA) na kusisitiza kuwa viongozi wa dini wakiwafundisha mema waumini ambao ndiyo wananchi Taifa halitakuwa na wahalifu au matukio ya wizi, ujambazi, utumiaji wa dawa za kulevya na ufanyaji wa biashara hiyo, jambo ambalo litaipunguzia gharama serikali ya kuwahudumia waathirika kwa kuwapa vidonge vya Methadone, na serikali haitatumia nguvu kubwa kujenga magereza kwa ajili ya wanaokiuka sheria na taratibu za nchi.
Pia, Makonda amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono viongozi wa dini kwani wanamchango mkubwa kwenye maendeleo ya Taifa hili.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa JUWAQUTA ambaye pia ni Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum amesema kuwa lengo la semina hiyo ni kuwaelimisha walimu hao juu ya kuunga mkono kauli mbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwani kufanya kazi ni agizo kwa mujibu wa dini hiyo ya kiislamu ambapo waumini wake wameambiwa wafanya kazi za halali ili wapate ridhiki halali na siyo vinginevyo.
Amefafanua kuwa hata manabii walikuwa wakifanya kazi, hivyo ni vyema kama viongozi kufuata nyayo hizo na kuwaamrisha wengine kufuata utaratibu huo.
Aidha, Mwenyekiti huyo wa JUWAQUTA alitumia wasaa huo kwa kujumika na viongozi wengine kumuombea Makonda ili aendelee kutimiza majukumu yake na Mwenyezi Mungu amlinde na mabaya.