Johansen Buberwa, Bukoba – Kagera.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi. Paul Makonda ametoa miezi mitatu kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa kutatua changamoto zinazowakabili Wananchi Mkoani Kagera, ikiwemo ujenzi wa Soko, Stendi ya Kimataifa na ujenzi wa kingo za mto Kanoni.
Makonda ametoa maagizo hayo katika uwanja wa Mayunga Mkoani Kagera, katika ziara yake ya Kanda ya Ziwa inayolenga kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Amesema, “Waziri Mchengerwa nakupa miezi mitatu uwe umekanyaga Kagera, nataka kuona mpango wa ujenzi wa Soko, tafuta pesa kokote Soko lijengwe, nataka kuona Stendi ya kisasa ya Kimataifa inajengwa Kagera pamoja na changamoto ya mto wa Kanoni imalizwe kwa kujenga kingo za mto huo.”
Awali akizungumza kwa niaba ya Wabunge wa Mkoa Kagera, Mbunge jimbo la Bukoba mjini Stephano Byabato amemshukru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za maendeleo na kumuomba mambo matatu ikiwemo fedha Bilioni 2.5 kwa ajiri ya kukamilisha ujenzi wa stendi ya Bukoba, Soko kuu na Bilioni 4 za kukamilisha ujenzi wa Barabara ya njia nne kutoka mtaa wa mitaga hadi stendi ya Bukoba.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Kagera Hajat. Fatuma Mwasa ameishukuru Serikali kwa uendelezaji wa utatuzi wa kero na changamoto za Wananchi na kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi na ukamilishaji wa miradi mbalimbali.