Katika kipindi cha robo ya tatu ya Mwaka wa Fedha 2022/23, Mamlaka ya Mapato Tanzania – TRA, imefanikiwa kukusanya Shilingi 5.9 Trilioni ambazo ni sawa na asilimia 97.9 ya lengo la kukusanya Shilingi 6 Trilioni.
TRA, imesema makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 6.1 ikilinganishwa na makusanyo ya kipindi kama hicho kwa Mwaka wa Fedha 2021/22 yakichangiwa na uboreshaji wa mifumo ya ukusanyaji kodi ambayo imerahisisha utaratibu wa ulipaji kodi kwa hiari.
Aidha, makusanyo hayo pia yamepatikana kutokana na kuongezeka kwa uwezo wa walipakodi katika kulipa malimbikizo ya kodi baada ya Serikali kuongeza kasi ya kulipa marejesho ya kodi.
TRA inasema sababu nyingine ni kuimarika kwa mahusiano baina ya Mamlaka na walipakodi ikiwemo utatuzi wa migogoro ya kodi nje ya Mahakama pamoja na kushughulikia malalamiko ya walipakodi kwa wakati.