Malezi ya Viongozi wa Dini kwa Vijana yamekuwa na mchango katika kulinda amani ya Taifa, kupunguza matukio ya uhalifu na kuimarisha huduma mbalimbali za kijamii na kuwataka kuhimiza Watanzania kuzingatia mila na tamaduni ili kuimarisha misingi ya maadili.
Hayo yamebainishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan hii leo Novemba 19, 2022 Jijini Dodoma wakati akitoa hotuba kwenye maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Utume na Huduma ya Kanisa la Waadventista Wasabato, Jimbo la Kati nchini.
Amesema, “Nimefurahishwa na kwaya mbili hapa, wameimba maudhui ya kizalendo na wamejengwa kizalendo. Kwa hiyo niwashukuru sana kwa malezi hayo, ni jambo jema sana kwani bila kuwa na vijana waadilifu, basi magereza yetu yangekuwa yamejaa.”
Hata hivyo, pia Rais Samia amelipongeza Kanisa hilo katika ushiriki wake wa kutoa huduma za kijamii kwenye sekta ya afya na elimu na kupongeza zaidi ya miaka 100 ya kuanzishwa kwa kanisa hilo.