Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi zimepewa siku saba kuhakikisha wanapata utatuzi wa changamoto inayokwamisha ujenzi wa barabara ya Pangani – Makurunge – Bagamoyo, ambayo imekwama kutokana na leseni ya eneo la jiwe la kuchimba kokoto kupewa mtu tofauti na mkandarasi.

Agizo hilo limetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango hii leo Novemba, 19 2022 wakati akizungumza na wananchi wa Mkata Wilaya ya Handeni mkoani Tanga akiwa safarini kuelekea Makao Makuu ya Mkoa huo, na pia kuagiza kutatuliwa mara moja changamoto iliokwamisha ujenzi wa barabara ya Handeni – Kibirashi – Kiteto hadi Dodoma ambayo ujenzi wake ulipaswa kuanza tangu mwezi Mei 2022.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango.

Amesema, Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) anatakiwa kuhakikisha wanafanyia kazi mapema maeneo yanayotumika kwaajili ya ujenzi wanayoyapata baada ya tafiti wanazofanya ili kuepusha migogoro inayokwamisha maendeleo ya miradi na kuwahimiza Wananchi wa eneo hilo juu ya utunzaji wa mazingira ikiwemo upandaji wa miti.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omary Mgumba alisema wataendelea kusimamia uhifadhi wa mazingira kwa kuchukua hatua kali zaidi ili kukabiliana na waharibifu na kwamba mkoa huo kwa sasa unakabiliwa na changamoto ya ukataji miti kwaajili ya uchomaji mkaa na baadhi ya viongozi katika maeneo ya vijiji na vitongoji wakishiriki katika biashara hiyo.

Aliyetawala tangu 1979 awania muhula wa sita wa Urais
Malezi kwa Vijana yachangia ulinzi amani ya Taifa