Rais mpya wa Mali ataapishwa leo ikiwa ni wiki tano baada ya kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa rais wa taifa hilo ambaye alipinduliwa na jeshi, Ibrahim Boubacar Keita.
Mapema wiki hii, kiongozi wa kijeshi ambaye aliongoza mapinduzi dhidi ya Keita, Assimi Goita alimteua waziri wa ulinzi wa zamani, Bah Ndaw ili kuongoza kama rais wa mpito mpaka uchaguzi utakapofanyika wakati yeye mwenyewe kanali Goita atakuwa makamu wa rais.
Serikali mpya inatarajiwa kuwa madarakani kwa kipindi cha mpito cha miezi 18, ambacho pia kitatumika kuandaa uchaguzi mkuu wa kidemokrasia wa taifa hilo.
Kuteuliwa kwa rais ambaye ni raia, kumefuatia juma lililopita jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika Magharibi yenye mataifa 15 wanachama ECOWAS kutoa siku kadhaa kwa watawala wa kijeshi wa Mali kuwateuwa viongozi wa kiraia, ikionya kwamba haitaviondoa vikwazo vyake endapo hatua hiyo haitotekelezwa.
ECOWAS iliiwekea Mali marufuku ya kibiashara na kufunga mipaka, katika kipindi ambacho kilizongwa na mapinduzi ya Agosti 18, ambayo yalimuondoa madarakani rais Keita ingawa kwa sasa Mali inatarajia tangazo kutoka kwa jumuiya hiyo baada ya uteuzi huu kukamilika.