Uchunguzi, uliochapishwa mapema Jumapili, na Jumuiya ya Kimataifa ya Wanahabari wa Upelelezi na mashirika mengine ya habari umeonesha kuwa Familia ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, ilimiliki kwa siri mtandao wa kampuni zilizofunguliwa katika maeneo yenye unafuu wa ulipaji ushuru kwa miongo kadhaa, kulingana na uvujaji wa nyaraka za kifedha.
Kenyatta na watu sita wa familia yake wamehusishwa na kampuni 13 zilizofunguliwa katika maeneo yenye unafuu wa ulipaji ushuru na bado hawajajibu ombi la kutoa maoni kuhusu ufichuzi huo.
Nyaraka zinaonyesha kwamba wakfu ulioitwa Varies ulianzishwa mnamo 2003 huko Panama, ukimtaja mama wa Kenyatta, Ngina, 88, kama mnufaika wa kwanza na Rais Kenyatta kama mnufaika` wa pili, ambaye angeurithi baada ya kifo cha mama yake.
Nyaraka za Pandora faili milioni 12 ndio kubwa zaidi iliyovuja katika historia na madhumuni ya wakfu huo na thamani ya mali yake haijulikani.
ICIJ inaripoti kuwa mashirika ya wakfu nchini Panama hutafutwa bila kufahamika kwa sababu wamiliki wa kweli wa mali wanajulikana tu na mawakili wao na sio lazima waandikishe majina yao kwa serikali ya Panama.
Hakuna makadirio ya kuaminika ya thamani halisi ya mali ya familia ya Kenyatta lakini shughuli zake kubwa za kibiashara zinasheheni kampuni katika sekta za uchukuzi, bima, hoteli, kilimo, umiliki wa ardhi na tasnia ya habari nchini Kenya.
Mnamo 2018, Kenyatta alinukuliwa na chombo cha habari mashuhuri cha kimataifa BBC kwamba utajiri wa familia yake unajulikana kwa umma, na kama rais alikuwa ametangaza mali zake kama inavyotakiwa na sheria.
“Ikiwa kuna mfano ambapo mtu anaweza kusema kuwa kile tulichofanya au kupata hakijakuwa halali, sema hivyo – tuko tayari kufika katika korti yoyote,” Kenyatta.
Viongozi wengine wa ulimwengu waliotajwa katika nyaraka za Pandora ni pamoja na Mfalme wa Jordan Abdullah II, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair, Rais wa Gabon Ali Bongo Ondimba na Rais wa Congo-Brazzaville Denis Sassou-Nguesso.