Mamlaka ya jimbo la Guateng nchini Afrika Kusini zimekanusha taarifa iliyoenea hivi karibuni ya Mwanamke aliyefungua mapacha kumi na kuvunja rekodi ya dunia ya Mwanamke aliyewahi kujifungua watoto wengi kwa mara moja.
Mamlaka hiyo imesema taarifa kuwa Gosiame Sithole alijifungua watoto 10 mapema mwezi huu sio ya kweli.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa hakuna hospitali yenye taarifa za watoto 10 kuzaliwa, na pia vipimo vimeonesha kuwa Sithole hakuwa mjamzito katika siku za karibuni bila kueleza sababu za mwanamke huyo kudanganya kuhusu ujauzito na kujifungua watoto hao na kwamba anapatiwa tiba ya kisaikolojia.
- Mama aliyejifungua mapacha 9 ashangaza wengi
- Wanajeshi wafariki dunia katika ajali ya helikopta Kenya
Hivi karibuni, Gosiame Thamara Sithole mwenye miaka 37 alisemekana kujifungua mapacha 10 na kuweka rekodi ya kipekee kwa kujifungua watoto kumi kwa siku moja katika Hospitali iliyosemekana kuwa jijini Pretoria bila hospitali hiyo kutajwa jina.
Mwandishi aliyechapisha habari hiyo kwa mara ya kwanza, Piet Rampedi huenda akachukuliwa hatua baada ya serikali kuagiza ofisi ya mwanasheria mkuu kumfungulia mashtaka ingawa Shirika la habari la mitandaoni linalomiliki Pretoria News na ambalo ndilo la kwanza kuripoti habari hiyo lilisimama kidete na kuunga mkono taarifa yake.
Ujauzito huo ulivutia hisia tofauti katika mitandao ya kijamii kote duniani na watu wakaanza kutuma ufadhili kwa wazazi wa watoto hao.
Hata hivyo, habari hiyo ilianza kutiliwa shaka baada ya Rampedi kushindwa kutaja hospitali ambayo watoto hao walizaliwa huku baadhi ya hospitali katika mkoa huo zikipinga madai kwamba mama huyo alikuwa amejifungua katika hospitali zao.
Iwapo taarifa za Gosiame ambaye anatokea Afrika Kusini kujifungua mapacha kumi sio za kweli, rekodi ya mwanamke aliyejifungua mapacha wengi inasalia kushikiliwa na Halima Cisse mwenye umri wa miaka 25 kutokea nchini Mali ambaye Aprili mwaka huu alijifungua watoto tisa.