Mabingwa wa Soka nchini England wameripotiwa kuanzisha mazungumzo na Mshambuliaji kutoka Norway Erling Braut Haaland kwa ajili ya kumsainisha mkataba mpya.
Haaland mwenye umri wa miaka 22, amekuwa akivunja rekodi za mabao kwenye Ligi Kuu England kama anavyotaka baada ya kufikisha mabao 50 katika michuano yote aliyochezea miamba hiyo ya Etihad msimu huu.
Sambamba na hilo, Haaland ameweka rekodi ya kufikisha idadi ya mabao 34, akivunja rekodi ya mabao kwenye Ligi Kuu England, akiwa mchezaji wa kwanza kufikisha idadi hiyo kwenye ligi yenye mfumo wa mechi 38.
Alan Shearer na Andy Cole waliwahi kufikisha idadi hiyo ya mabao 34 ndani ya msimu mmoja wa Ligi Kuu England, lakini kwa wakati huo mechi zilikuwa 42.
Licha ya Haaland kusaini mkataba wa miaka mitano alipotua Man City mwaka jana, lakini miamba hiyo ya Etihad inahitaji aendelee kubaki kwenye kikosi hicho kwa muda mrefu walau hadi 2029.
Baada ya kutua Etihad kwa Pauni 52.6 milioni kutoka Dortmund mwaka jana, Haaland inaaminika kwamba kwenye mkataba wake kuliwekwa kipengele kinachoruhusu dili hilo kuvunjwa kwa Pauni 150 milioni tu itakapofika 2024.
Na sasa, Man City wanataka kumpa mkataba mpya ili kukiondoa kipengele hicho kisifanye kazi kuwatibulia Real Madrid wanaopiga hesabu za kwenda kumsajili mchezaji huyo.
Mkataba wake wa sasa utafika mwisho 2027, lakini wanataka kumwongezea miaka miwili ili aendelee kubaki Etihad hadi 2029.