Msemaji wa Klabu ya Simba, Haji Manara amewatumia ujumbe mashabiki wa klabu hiyo kuhusu mchezo wa watani wao Yanga dhidi ya Township Rollers kutoka Botswana utakaoshuhudiwa kesho, Agosti 10, 2019 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikiwa ni mchezo wa hatua ya kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Manara ameandika kupitia Instagram akiwataka mashabiki wa Simba kuangalia Utanzania kwanza katika mechi za kigeni, kwani ni timu nne pekee nchini ambazo zina nafasi ya kupeperusha bendera ya Tanzania katika makombe ya kimataifa wakati huu.

Ameandika:

“Imetuchukua miongo kadhaa kama nchi kupata fursa ya kuwakilishwa na vilabu vinne Kwenye Mashindano ya CAF. Ni @simbasctanzania wenye mchango mkubwa sana ktk hili!! Kama Taifa tunatakiwa tufanye vizuri zaidi kupitia wawakilishi wetu ili tuendelee kwa miaka ijayo kuwa na klabu nne ktk CAF Competitions!! Najua ni ngumu kunielewa leo , lakini nawaomba Wanasimba wote kesho msizomee @Yangasc ,msilipe kisasi na wekeni maslahi mapana ya nchi,sisi ni waungwana na uungwana ni vitendo!! Kama hujiwezi usiende Taifa na ikibidi kwenda na huwezi kuwashangilia bora ukae kimya!!

Najua walitukera msimu uliopita lakini tuiangalie nchi kwanza na pia tujue wao, @azamfcofficial na @kmcfc_official pamoja na cc ndio tuna nafasi ya kuendelea kupewa nafasi nne tena msimu ujao!! Pls watu wangu nieleweni ktk hili, Naiangalia Tanzania kama nchi,utani na kuzodoana kwetu utatugharimu sote,kama kuwacheka tuwacheke baadae lakini kwa sasa interest ya Tanzania iwe moja ???,” -Haji Manara.

Katika hatua nyingine, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Dismas Ten amesema kuwa timu hiyo imejipanga kupata ushindi ikiwa nyumbani na kufuta makosa iliyofanya mwaka jana ilipopigwa 2-1 na Rollers katika hatua kama hii.

“Tuna mtazamo chanya kuelekea mechi ya wikendi hii, tunakiri kuwa ni mechi kubwa lakini timu iko tayari,” alisema Ten.

“Tuko tayari… huu sio msimu uliopita, walitupiga msimu uliopita lakini ni wakati wetu kusahihisha makosa na kuwaondoa,” aliongeza.

Mbali na Yanga, timu nyingine tatu za Tanzania ziko katika michuano ya kimataifa wakati huu, Simba wakishiriki pia Ligi ya Mabingwa Afrika. Azama na KMC FC wao waashiriki Kombe la Shirikisho  la CAF.

Video: Willy Paul, Ali Kiba na Ommy Dimpoz waachia ‘Nishikilie’, iangalie hapa
Mabula azungumzia hasara ya mabilioni, 138 wa wizara walioburuzwa Takukuru