Klabu ya Manchester City kwa sasa iko katika kiwango cha juu sana na ni wazi kwamba kwa sasa hakuna asiyeigopa kwani katika michezo 10 tayari wana alama 28 ikimaanisha wamepoteza alama 2 tu hadi sasa.
Man City watakuwa nyumbani leo kwenye uwanja wa Etihad Stadium kuwakabili Arsenal na kama Pep Guardiola ataifunga Arsenal hii leo baasi atafikia rekodi ya Manchester City waliyoweka mwaka 1947 ya kushinda michezo 9 mfululizo katika msimu mmoja wa ligi.
Tayari Manchester City wamefunga jumla ya mabao 35 msimu huu rekodi ambayo inawatishia sana wapinzani wao huku Arsenal hadi sasa wakiwa wamefunga mabao 19 tu katika ligi kuu Uingereza.
Arsenal hawapewi nafasi ya kuibuka na ushindi katika mchezo wa leo lakini ukweli ni kwamba katika michezo 9 ambayo Man City wamekutana na Arsenal, City wameshinda mara moja tu tena ilikuwa msimu uliopita pale Etihad.
Kama Arsenal watafungwa katika mchezo wa leo baasi watakuwa wamepoteza mchezo wao wa nne ugenini na hii itakuwa mara ya kwanza kupoteza michezo 4 kati ya 6 ugenini tangu mwaka 1981.
Kocha Arsene Wenger ana jambo la kujigamba hii leo kwani ndio kocha pekee ambaye amewahi kumfunga Pep Gurdiola akiwa Barcelona, Bayern Munich na Manchester City.