Mapigano yalizuka kwenye mpaka wa eneo la Tigray hapo jana Agosti 24, 2022, na kuhitimisha usitishaji mapigano wa miezi mitano kati ya waasi na serikali ya nchini Ethiopia.
Waasi wa Tigrayan, serikali ya Ethiopia na wakazi wa eneo hilo, walithibitisha kuwa mapigano yalikuwa yanatokea karibu na eneo la Kobo, mji uliopo kaskazini mwa Ethiopia, kufuatia wiki kadhaa za msururu wa kijeshi katika pande zote zinazoshutumiana kuanzisha mashambulizi.
Mapigano hayo, yalizua hofu kuhusu wimbi jingine la ghasia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoharibu mahusiano, ambavyo vinaweza kuhatarisha watu milioni sita ambao tayari wamekwama katika maafa ya kibinadamu duniani huku wengi wao wakiwa kwenye njaa kali.
Mzozo huo wa Tigray, ulianza Novemba 2020 wakati ambapo Serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed ilikataza ufikiaji wa eneo hilo Julai 2021, baada ya waasi wa Tigrayan kuwafukuza wanajeshi wa serikali, na kupata ushindi wao wa kwanza.
Hata hivyo, hali ya utulivu imetawala tangu mwezi Machi 2022, wakati pande zote mbili zilikubali makubaliano ya kuruhusu misaada ya kibinadamu kuwasilishwa itakayosaidia raia wasio na hatia kupata huduma za kijamii.
Shirika la Habari la Ethiopia (ENA), hapo jana liliripoti kuwa Jeshi la nchi hiyo liliidungua ndege iliyokuwa na silaha zilizokuwa zikipelekwa kwa waasi wa Tigray, ambayo ilikiuka taratibu za anga ya Ethiopia, iliyokuwa ikipita jirani na anga la nchi ya Sudan.