Serikali nchini, imejipanga kuanzisha mpango wa ufugaji nyuki ujulikanao kama Manzuki, watakaokuwa wanafugwa katika eneo maalum bila kuathiri uhifadhi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Uyovu, iliyopo Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita.

Amesema, kupitia mpango huo wananchi wataweza kufuga nyuki na kupata faida bila kuhama kuhama kama ilivyozoeleka kwa wale wa asili.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja (wa tatu kutoka kulia), Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela (wa nne kutoka kulia), Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa pili kutoka kulia) pamoja na viongozi wa Serikali na chama wakiwa katika mkutano na wananchi wa Kata ya Uyovu Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita kuhusu masuala ya uhifadhi na ufugaji nyuki.

Kuhusu wananchi wanaofuga nyuki katika Hifadhi ya Kigosi, amesema kuwa Serikali imeruhusu wananchi kuendelea na shughuli za ufugaji nyuki wakati inatafuta eneo mbadala la kuwahamishia wafugaji hao.

“Tamko la Serikali ni kwamba shughuli za ufugaji nyuki zitaendelea hadi pale tutakapotoa mbadala wa wapi mpeleke mizinga yenu.” Masanja amesisitiza.

Aidha, amewataka wananchi kukitumia ipasavyo Kiwanda cha kuchakata asali kilichopo katika eneo hilo, ili waweze kuuza asali kwa faida na kuwasisitiza kuhusu suala la utunzaji wa mazingira na kuacha kukata miti hovyo ili kuendelea kufaidika na mazao ya nyuki.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja (atikati), akisikiliza maelezo ya namna mitambo ya kiwanda cha kuchakata mazao ya nyuki inavyofanya kazi, katika Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela pamoja na viongozi na watendaji wa Serikali.

Awali, Waziri wa Madini na mbunge wa jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko amesema, Rais Samia anataka kuona kero za wananchi wakiwemo wa Uyovu zinatatuliwa na ndiyo maana Naibu Waziri amefika, hivyo wananchi wawe wahifadhi kwa kuilinda misitu ya Bukombe isiharibiwe.

Naibu Waziri, Mary Masanja anaendelea na ziara yake katika Kanda ya Ziwa kwa lengo la kusikiliza na kutatua changamoto zinazoikabili Sekta ya Maliasili na Utalii.

Hassan Mwakinyo auota mkanda wa WBO
Mapigano yazuka upya jirani na eneo la Tigray