Marais kutoka nchi 10 barani Afrika, pamoja na waliostaafu wameshiriki mazishi ya Rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe yaliyofanyika leo Jumamosi Septemba 14, 2019.
Mwili wa mwanamapinduzi huyo aliyefariki Septemba 6, 2019 nchini Singapore alipokuwa akipatiwa matibabu umeagwa leo katika uwanja wa Harare.
Marais walioshiriki ni Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta; Rais wa Zambia, Edgar Lungu; Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi; Rais wa Namibia, Hage Geingob; Rais wa Equatorial Guinea, Teodoro Mbasogo; Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa; Rais wa Madagascar, Andry Rajoelina; Rais wa Malawi, Peter Mutharika; Rais wa Angola, João Lourenço na Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, Rais wa Singapore, Halimah Jacob, huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwakilishwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu.
Mugabe amekuwa kiongozi wa Zimbabwe toka 1980 mpaka 2017. Alikuwa Waziri Mkuu hadi 1987 alipochukua usukani kama rais wa nchi hiyo, na mwishowe kung’olewa kwa msaada wa jeshi.
Utawala wake awali ulisifiwa kwa kuinua maisha ya raia na kukuza uchumi lakini mwishowe ulishutumiwa kwa ukandamizaji wa upinzani, ukiukaji wa sheria za uchaguzi, na kusababisha uchumi wa nchi kuanguka.