Mwanasheria Mkuu wa Marekani, William Barr amewaamuru waendesha mashitaka wa serikali kuanzisha uchunguzi kuhusu dosari za upigaji kura, kwa sababu Rais Donald Trump amedai kuwa alishindwa uchaguzi kutokana na udanganyifu.
Barr, ambaye ni mtetezi wa karibu wa Trump kwa muda mrefu, amesisitiza barua yake kwa wanasheria wa Marekani sio ishara ya kuwa Wizara ya Sheria ina ushahidi kwa matukio udanganyifu.
Uchunguzi wa udanganyifu katika upigaji kura kawaida hufanywa na majimbo binafsi, ambayo huweka na kuchunguza kanuni zao za uchaguzi.
Amri ya Barr imekuja wakati Trump akipambana kuubatilisha ushindi mwembamba wa mpinzani wake toka chama Democratic Joe Biden katika majimbo ya Pennsylvania, Nevada, Georgia, na Arizona ambayo yalimpa asilimia kubwa ya kura za wajumbe ili kushinda uchaguzi wa rais kwa ujumla.