Ubalozi wa Marekani nchini Kenya, umewataka viongozi wa pande zote mbili nchini humo kutatua kwa amani wasiwasi wowote uliosalia kuhusu uchaguzi huo, kupitia taratibu zilizopo za kutatua mizozo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa imesema, wanapongeza juhudi za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, vikosi vya usalama, na taasisi zote za uchaguzi kuandaa utaratibu wa amani na utulivu wa upigaji kura na kuhesabu kura.
Chini ya uongozi wa Mwenyekiti Wafula Chebukati, IEBC hapo jana ilimtangaza William Ruto kuwa mshindi wa kiti cha urais.
Aidha, Ubalozi huo umewataka viongozi wote wa vyama vya siasa kuendelea kuwasihi wafuasi wao kuendelea kuwa watulivu na kujiepusha na vurugu.
Ubalozi wa Marekani, ulipongeza ushiriki mkubwa wa vyama vya siasa vya Kenya, mashirika ya kiraia, na raia katika kuunda mijadala dhabiti katika kipindi chote cha kampeni.
“Marekani na Kenya zina ushirikiano na historia ya kufanya kazi pamoja kwa kuboresha huduma za afya, kukuza amani na usalama katika eneo hili, kuendeleza heshima ya haki za binadamu, na kuimarisha uchumi wetu na tunatazamia kuendelea kuimarisha ushirikiano wetu na watu na serikali ya Kenya,” imesema taarifa hiyo.